RC Hapi asimikwa uchifu wa Wahehe

Na Herieth Rebman | Agosti 11, 2018

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Ally Salum Hapi leo amefanya mkutano na wazee wa Mkoa wa Iringa na kusimikwa rasmi kuwa Chifu wa kabila la Wahehe ikiwa ni ishara ya kumpokea na kumpa nguvu ya kuutawala mkoa huu.

Katika mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, RC Hapi aliwasilisha kwa wazee hao salamu za Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli na baadaye kutoa hotuba ya dira ya uongozi wake, vipaumbele vyake pamoja na kuwaomba ushirikiano wananchi wa Iringa.

“Mhe Rais amenituma niwape salamu zake. Lakini pia amenipa kazi ya kuhakikisha tunawatumikia na kutatua kero zenu ili wanaIringa mjivunie kuwa hamkukosea kumchagua Rais Magufuli na mjisikie fahari na nchi yenu. Siku zote nitasimama upande wenu wananchi na hasa wanyonge…”, alisema Hapi

Katika hatua nyingine RC Hapi alitoa fursa kwa wazee hao kueleza matarajio yao na changamoto zao ambazo wangependa serikali ya mkoa izifanyie kazi.

Aidha, wazee wamemueleza RC Hapi changamoto za huduma zisizoridhisha katika hospitali ya Mkoa wa Iringa ikiwa ni pamoja na majibu mabaya ya watoa huduma, halikadhalika migogoro ya ardhi na maji, mikopo ya kina mama pamoja na ucheleweshwaji wa pembejeo kwa wakulima.

Wazee hao wakiongozwa na Kaimu Chifu wa Wahehe Mzee Gerald Malangalila pia wameeleza mkutano huo kuwa ni wa kihistoria kuwahi kutokea mkoani Iringa.

“Haijawahi kutokea kwa miongo mingi kiongozi akapokelewa kwa umati mkubwa wa wazee kama huu hapa kwetu. Hii ni dalili kuwa kama ilivyo kwa Rais, nawe umeletwa na Mungu. Sasa tumekutawaza kuwa Chifu wetu, tutakutii, tutakupa ushirikiano na tutakulinda”, alisema Chifu Malangalila

Akitoa neno la shukrani Mzee Agustino Mkini ambaye ni Mwenyekiti wa baraza la wazee wa mkoa wa Iringa, alimshukuru Mkuu wa Mkoa na kumuahidi ushirikiano katika kujenga Iringa Mpya.

“Tunamshukuru sana Mhe Rais kwa kukuleta Iringa. Tunataka yale uliyokua unayafanya Kinondoni tukikuona, uyafanye Iringa…”