Mwanadiplomasia wa Marekani azuru Country FM

Na Mweha Msemo I Novemba 1, 2018

Ikiwa Country FM ni miongoni mwa wanufaika wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ya Marekani hapa nchini, mmoja wa wanadiplomasia wa juu katika ubalozi wa nchi hiyo hapa Tanzania alifanya ziara ya siku moja katika kituo hiki ikiwa ni hatua za kufuatilia utekelezaji wa miradi husika. Chini ni maelezo mafupi kutoka kwa mwandiplomasia huyo katika tafsiri la lugha ya Kiswahili.

Jina langu ni Brinille Ellis. Mimi ni mwanadiplomasia wa Marekani; ninafanya kazi Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania. Mimi ni Mkuu wa kitengo cha Mahusiano ya Umma ambacho kina jukumu la kusimamia mahusiano ya vyombo vya habari, utamaduni na elimu kati ya Marekani na watu wa Tanzania.

Nimekuwepo Tanzania kwa zaidi ya mwaka mmoja na nimekuwa mwanadiplomasia kwa miaka ishirini na moja. Nimekuwa Iringa kwa siku mbili sasa kujifunza zaidi kuhusu ushiriki na kujitoa kwa serikali ya Marekani kwa Watu wa Tanzania kupitia miradi yake mingi inayojikita katika kuboresha afya, elimu, maendeleo, kilimo pamoja na amani na ulinzi wa Watanzania.

Tanzania ikifanikiwa tunafanikiwa sote. Serikali ya Marekani inashirikiana na Watanzania katika nyanja mbalimbali ikiwa eneo kubwa zaidi la juhudi zetu ni afya. Mwaka huu tunasherehekea miaka 15 ya mpango ulioanzishwa na Rais George W. Bush, yaani Mpango wa Rais wa Kushugulikia Masuala ya UKIMWI, tunaouita PEPFAR. Tangu mwaka 2003 serikali ya Marekani imetumia kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 4.5 nchini Tanzania ili kusaidia kutokomeza UKIMWI, lakini pia katika matibabu na elimu ili kuboresha maisha ya Watanzania.

Siku chache zilizopita nimekutana na wadau wetu wa afya, watafiti pamoja na wanufaika wa elimu ya kuishi na maambukizi ya virusi vinavyosababisha UKIMWI, vilevile wanufaika wa matibabu. Hatujamaliza, bado tuna kazi kubwa ya kufanya kwani tunalenga kufikia hatua ya kutokuwa kabisa na maambukizi, vifo na unyanyapaa. Hii ni kujifunza kwamba kuishi na virusi vinavyosababisha UKIMWI siyo hukumu ya kifo.

Idara yangu ya Mahusiano ya Umma inashirikiana na jamii ya Watanzania, na tunafanya hivyo katika nyanja mbalimbali hususani katika mipango ya ubadilishanaji uzoefu. Tuna mipango mingi inayotoa fursa kwa Watanzania kwenda Marekani kuimarisha taaluma zao na kujifunza kutoka kwa Wamarekani waliomo katika taaluma zinazohusiana na afya na mahusiano ya kimataifa ili kuzijenga jamii zao.

Zimekuwa siku mbili nzuri sana hapa Iringa, pia nimetembelea Chuo Kikuu cha Iringa na kujifunza kuhusu masomo na taaluma mbalimbali wanazotoa, lakini pia utamaduni wa Iringa na watu wake wazuri.

Brinille Ellis, Mkuu wa kitengo cha Mahusiano ya Umma kutoka Ubalozi wa Marekani (wapili toka kulia) akiwa katika ofisi za Country FM. Wakwanza kulia ni Afisa kutoka Ubalozi huo katika picha ya pamoja na meneja wa Country FM Bi. Chiku Mbilinyi (wapili kutoka kushoto) pamoja na Mkuu wa dawati la habari wa redio hiyo..

Ahsanteni kwa ukarimu wenu, na ninatarajia kurudi tena Iringa!

Kwa taarifa zaidi kuhusu miradi na shuguli zinazotekelezwa na Serikali ya Marekani hapa Tanzania, nawahimiza kutembelea tovuti yetu na kurasa zetu katika mitandao ya kijamii.