Mchungaji Msigwa awapa mkakati wabunge Iringa

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amewataka wabunge wa Iringa kuungana kupiga kelele ili Serikali ijenge barabara ya lami kutoka Iringa kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Akizungumza leo Alhamisi Februari 14, 2019 katika kikao cha bodi ya barabara mkoani Iringa, Mchungaji Msigwa amesema barabara hiyo ikiwekwa lami itafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi. “Tukiweka itikadi za vyama vyetu pembeni tukaungana wote kuipigia kelele Serikali ijenge barabara hii na ikajengwa itafungua fursa za utalii na kuongeza kipato kwa wananchi kuliko sasa watalii wanakuja kwa kusuasua,” amesema Mchungaji Msigwa.

Wakati Msigwa akieleza hayo mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa amesema Wakala wa Barabara (Tanroads) wana mpango gani wa kujenga barabara hiyo kwa kuwa tayari Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipokwenda mkoani humo, aliagiza iwekwe lami.

Chanzo: Mwananchi