Iringa yang’ara kwa usafi kitaifa

Na Herieth Rebman | Novemba 23, 2018

Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeshika nafasi ya kwanza Kitaifa katika mashindano ya usafi na mazingira nchini.

Iringa imetangazwa kushinda Leo katika kilele cha wiki ya usafi na mazingira duniani, sherehe zilizofanyika ukumbi wa Julius Nyerere mjini Dodoma na mgeni rasmi wa shehere hiyo akiwa Waziri mkuu Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa.

Kutokana na Ushindi huo Manispaa ya Iringa imekabidhiwa Trekta jipya baada ya kushinda nafasi hiyo ya kwanza.

Akihutubia katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu Mh Majaliwa amewataka wakurugenzi kote nchini kujifunza kutoka kwa halmashauri zilizofanya vizuri katika usafi wa mazingira.

Pia ameagiza kila halmashauri kujenga vyoo katika barabara ili kuepusha wasafiri kuchafua mazingira kwa “kuchimba dawa” njiani hovyo.

Aidha ametaka maafisa afya kuelekeza ukaguzi wa vyoo katika nyumba za ibada na maeneo yenye mikusanyiko ya watu.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Alex Kimbe amesema ushindi huo ni heshima kubwa kwa halmashauri ya Manispaa ya Iringa na Mkoa kwa ujumla .

Kwani amesema kwa Mkoa wa Iringa ni Manispaa ya Iringa pekee ambayo imeweza kuubeba Mkoa katika mashindano hayo na kuwa hii si Mara ya kwanza kwa Manispaa hiyo kufanya vizuri . Hivyo amewataka wananchi wa Manispaa ya Iringa kuendelea kufanya usafi katika mazingira yanayowazunguka pamoja na kuwa na vyoo bora.