Hali uwanja wa Nduli hairidhishi: RC Hapi

Na Philberta Kabonyela |Septemba 5, 2018

Mkuu wa mkoa wa Iringa Mh. Ally Hapi emeeleza kutoridhishwa na hali halisi ya uwanja wa ndege wa Nduli uliopo kata ya Nduli mkoani hapa katika kufanikisha maendeleo stahiki kwa manufaa ya wakazi wa mkoa wa Iringa.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua ukarabati mdogo unaoendelea katika uwanja huo, Mh. Hapi alisema kuwa uwanja huo wa ndege unahitaji ukarabati wa kiwango cha juu ili kukidhi mahitaji ya watumiaji ili kuwezesha ustawi wa maendeleo kwa wananchi wa mkoa huu.

“Nimetembea kwenye maeneo mengi ya uwanja huu na nimeona hayaridhishi wala kuvutia kwa wawekezaji kufika hapa mkoani; awawekezaji wengi wanapendelea zaidi kutumia usafiri wa anga, hivyo ni lazima kuwa na kiwanja cha ndege ambacho kitakidhi na kuvutia watalii na wawekezaji wanapokuja mkoani hapa”, alisema Hapi Hapi alisema kuwa jengo la wasafiri uwanjani hapo ni dogo na lisilo na ubora unaotakiwa na pia halikidhi kuwa sehemu ya uwanja huo ambao hivi karibuni unatarajiwa kuanza kupokea wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali ya ndani ya nje ya nchi.