Country FM yanufaika uwezeshaji Internews, USAID

Na Herieth Rebman | Februari 22, 2019

Katika juhudi za kuboresha maudhui kwa vyombo vya habari vya Tanzania, shirika la Internews kupitia mradi wa USAID Boresha Habari wametoa vitendea kazi mbalmbali kwa radio jamii 19 huku Country FM ikiwa ni moja ya vituo vilivyonufaika.

Zoezi la ugawaji vifaa lilifanyika Jijini Dar es salaam mara baada ya kumalizika mkutano wa siku 3 wa Radio Jamii washirika wa Internews kupitia mradi wa Boresha Habari uliolenga kuzungumzia masuala ya Masoko.

Akikabidhi vifaa hivyo mkurugenzi wa shirika la maendeleo la Marekani (USAID) nchini Tanzania Bw. Andy Karas alisema, Marekani itaendelea kuunga mkono uhuru wa vyombo vya habari katika kuhakikisha vinafanyakazi kwa uhuru na weledi ili kutatua matatizo yanayowakabili watanzania.

Kwa upande wake mkurugenzi wa habari na mawasiliano katika shirika la Internews, Wenceslaus Mushi alieleza umuhimu kwa vyombo vya habari kuwa na maudhui yenye utofauti na bora ili kuwafikia wasikilizaji wao na habari zinazowahusu ili vituo hivyo kuweza kukua kiuchumi.

Naye mshauri wa biashara kwa vyombo vya habari Justice Lutenge alisema kuwa ili vyombo vya habari viweze kufanikiwa katika masoko lazima vijiwekee makadirio yenye mikakati ili kufikia wateja wao na kuweza kukidhi melengo ya kuanzishwa kwa vyombo hivyo.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya uongozi meneja wa kituo hiki Bi Chiku Mbilinyi alisema mradi wa Boresha Habari umekuwa msaada mkubwa kwao kwani kwa sasa kituo chake kimeanza kufanya vizuri kibiashara ikilinganishwa na hapo awali.

Pichani ni Bi. Herieth Rebman Molla (aliyesimama), mwandishi wa habari na mtangazaji wa redio Country FM akichangia mada wakati wa mafunzo yalioandaliwa na Internews in Tanzania kupitia mradi wa USAID-Boresha Habari

Pichani ni wanahabari kutoka radio jamii mbalimbali wakiwemo Bi. Chiku Mbilinyi (mwenye blauzi ya machungwa) na Bi. Herieth Molla (mwenye gauni la kitenge) ambao ni wawakilishi toka Country FM. Wanahabari wamejadili kwa pamoja masuala mbalimbali katika mafunzo hayo ya siku tatu yaliondaliwa na taasisi ya kimataifa ya Internews kupitia mradi wa USAID-Boresha Habari yaliyolenga ‘kuwanoa’ kitaaluma.

Kimsingi, ipo sababu ya kutambua na kujali juhudi zinazofanywa na wanahabari. Hii ni pamoja na kuwapatia fursa za muhimu ili kuweza kuutumikia umma, halikadhalika na mafunzo ya mara kwa mara wawapo kazini. Kuna umuhimu wa kuboresha tasnia hii kwa njia ya mafunzo ili kuendelea kuwa mchango muhimu kwa ustawi wa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Picha zote na: Internews in Tanzania