Changamoto sekondari ya Kiponzelo zaiteteresha taaluma

Na Philberta Kabonyela | Machi 5, 2019

Baadhi ya changamoto zinazopatikana katika shule ya Sekondari Kiponzelo wilayani Iringa mkoani hapa zimeelezwa kusababisha kushuka kwa taalumaa katika shule hiyo.

Akizungumza na redio Country FM, makamu wa bodi ya Shule ya Sekondari Kiponzelo amesema kuwa shule hiyo imekuwa ikikabiliana na changamoto kadhaa ikiwamo upungufu wa madawati kufuatia ongezeko la wanafunzi kutoka kata za jirani jambo linalosababisha wanafunzi hao kukalia ndoo.

Aidha ameeleza kuwa shule hiyo inakabiliwa na upungu wa vyumba vya madarasa pamoja na matundu ya vyoo jambo linalosababisha ugumu katika kuendesha shughuli mbalimbali za kitaaluma shuleni hapo.

Pia makamu huyo amesema kuwa ongezeko la wanafunzi katika shule hiyo limesababisha ukosefu mkubwa wa mabweni na hivyo kushamiri kwa changamoto za wanafunzi kutafuta makazi katika maeneo yasiyo salama nje ya shule.

Nao wananchi wa kijiji cha Kiponzelo wameeleza kuwa changamoto shuleni hapo zimesababisha kushuka kwa taaluma ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Hata hivyo, wananchi hao wameiomba serikali ya mkoa wa Iringa kufika shuleni hapo ili kuweza kuziona changamoto hizo na kuzitatua kwa uharaka ili shule hiyo iweze kuendelea kufanya vizuri kitaaluma.